Tuesday, 2 June 2015


Kilabu ya Manchester United inaamini iko katika nafasi nzuri ya kumsajili Dani Alves kutoka Barcelona iwapo kocha Louis Van Gaal anataka kumsajili beki huyo wa kulia.
Alves atakuwa hana mkataba mwishoni mwa msimu huu na Barcelona iko tayari kumwachilia beki huyo wa miaka 32 kuondoka baada ya mechi ya fainali ya vilabu bingwa Ulaya dhidi ya Juventus siku ya jumamosi mjini Berlin.
Klabu ya PSG pia inamuania Alvez ijapokuwa kocha wake Laurent Blanc anaamini mchezaji huyo bado anataka kusalia Barcelona.
Lakini maoni ya Old Trafford ni kwamba Alvez hangependelea kujiunga na PSG.
Dani Alves
Van Gaal anapanga kumsajili beki wa kulia.Licha ya umri wake mkubwa ukosefu wa fedha za uhamisho zinamfanya mchezaji huyo kuwa muhimu.
Mchezaji huyo wa Brazil anapokea kitita cha pauni 120,000 kwa wiki, fedha ambazo United inaweza kuzilipa bila kutoa jasho.

Shirikisho la kandanda duniani,FIFA, limekanusha madai kwamba katibu wao mkuu,Jerome Valcke,alihusika katika kashfa ya ufisadi ambapo hongo ya mamilioni ya dola ilitolewa.
Kashfa hiyo inachunguzwa na Marekani .
FIFA inasema hamna afisa wake yeyote wa ngazi ya juu aliyehusika kwa njia yoyote katika kashfa hiyo.
Jerome Valcke
Inasemekana malipo hayo ya rushwa yalitolewa na serikali ya Afrika Kusini kwa maafisa wa soka wa huko Marekani ili waunge mkono wenzao Waafrika walio ng'ambo katika nchi ya visiwa vya Caribbean.
Waendesha mashtaka wa Marekani wanasema hongo hiyo ilinuiwa kusaidia kununua kura kuiwezesha Afrika Kusini kuwa mwenyeji wa kombe la dunia lililofanyika mwaka 2010.

Wanamgambo wa kiislamu nchini Nigeria wametoa picha mpya za video lakini Kiongozi wa Boko Haram ambaye huwa anaonekana kwenye video zao, Abubakar Shekau hakuonekana kwenye picha hizo za video.
kutoonekana kwa Shekau kwenye Video hiyo kumeleta hali ya wasiwasi kuhusu kuwepo kwa hali ya mgawanyiko ndani ya kundi hilo.
Takriban watu 13 wameuawa siku ya jumanne katika shambulio la bomu katika Soko la Ng'ombe mjini Maiduguri, mji ambao uliwahi kuwa ngome ya Boko Haram, Kaskazini mashariki mwa Nigeria.
Katika picha ya video ya dakika 10, msemaji huyo amekanusha taarifa zilizotolewa na Jeshi la Serikali kuwa linadhibiti miji yote kutoka mikononi mwa wanamgambo.
Ameonyesha vitambulisho vya wanajeshi akisema kuwa wameuawa, na kuonyesha mabaki ambayo amedai ya ndege ya kijeshi waliyoidungua.
Msemaji aliyekuwa amebeba bunduki na huku uso wake ukiwa umefunikwa, amesema video hiyo ilirekodiwa sambisa, msitu unaozunguka hifadhi.
Rais wa Nigeria, Muhammadu Buhari,amesema kuwa vikosi vya kijeshi viko kwenye doria mjini Maiduguri na kuhakikisha kuwaondoa wanamgambo hao katika eneo hilo.
Baadae wiki hii, Buhari atakutana na Viongozi wenzie wa nchi jirani kwa ajili ya kuzungumzia mikakati ya kijeshi dhidi ya wanamgambo wa kiislamu.
Takriban watu milioni moja na nusu wamekimbia makazi yao, na mamia zaidi wametekwa tangu kuanza kwa harakati za kundi hilo mwaka 2009.
Zaidi ya Watu 15,500 wameuawa katika mapigano.
Rafael Nadal bingwa mara tisa wa michuano hiyo anavaana na Djokovic mchezaji nambari moja kwa ubora. Nadal Mhispania amewahi kumshinda Mserbia Djokovic mara sita katika michuano hiyo siku za nyuma.
Huu unaelezwa kuwa mpambano mkali zaidi katika michuano ya French Open inayoendelea katika viwanja vya tenis mjini Paris ukiwemo uwanja wa Roland Garros.
Rafael Nadal
Mchezaji nambari mbili kwa ubora katika mchezo huo duniani kwa wanaume na bingwa wa mwaka 2009 Roger Federer ameng'olewa katika michunao hiyo hatua ya robo fainali baada ya kucharazwa na Stan Wawrinka kwa seti 6-4 6-3 7-6 (7-4).
Wawrinka, mwenye umri wa miaka 30, amewahi kupoteza michezo yote minne walipokutana na Federer katika michuano hiyo mikubwa.
Lakini Wawrink ambaye ni wa nane kwa ubora katika tenis amemwangusha Federer mwenye umri wa miaka 33 ambaye alikuwa mchezaji mwenza katika michuano ya Kombe la Davis.
Andy Murray
Kwa matokeo hayo Wawrinka atapambana hatua ya nusu fainali na Mfaransa Jo-Wilfried Tsonga ambaye anapewa nafasi kubwa kufuatia ushindi wake dhidi ya Mjapan Kei Nishikori.
Tsonga alipata kibarua kigumu kumng'oa mpinzani wake Nishikori alipopata matokeo ya kufunga seti tatu dhidi ya mbili yaani 6-1 6-4 4-6 3-6 6-3.
Kwa upande mwingine Andy Murray leo atajaribu kutinga hatua ya nusu fainali ya michuano ya French Open kwa mara ya tatu katika siku ambayo Novak Djokovic na Rafael Nadal wanapambana mjini Paris.
Murray wa tatu kwa ubora duniani anacheza dhidi ya Mhispania David Ferrer anayeshika nafasi ya saba kwa ubora.
Murray amesema hilo litakuwa pambano kali na mtihani mkubwa kwake.

Waziri wa Usafirishaji wa China amesema wafanyakazi wa vikosi vya uokoaji wanafanya kila jitihada kuhakikisha wanawapata watu walionusurika miongoni mwa mamia ya waliokumbwa na mkasa wa kuzama kwa meli katika mto Yangtze kutokana na hali mbaya ya hewa.
Maelfu ya waokoaji walifanya kazi usiku kucha katika meli hiyo iliyopinduka ijulikanayo kama "Nyota ya Mashariki" katika jimbo la Hubei.
Watu saba wamethibitika kufa na wengine 14 wamekutwa hai katika meli hiyo iliyokuwa na watu 456.
Ndugu waliojawa na hasira wanalalamikia kukosekana kwa taarifa za uokoaji.
Watu walionusurika ni pamoja na nahodha wa meli na mhandisi mkuu, wote wawili wakiwa katika mahabusu za polisi.
Nahodha amesema meli hiyo ilikumbwa na kimbunga na kuzamishwa chini ya mto katika dakika chache.

Imeripotiwa kuwa Raisi wa Fifa,Sepp Blatter anafanyiwa uchunguzi na maafisa wa marekani ili kuthibitisha tuhuma za rushwa zinazomkabili vyombo vya habari vya Marekani vimeripoti.
Taarifa hiyo inakuja baada ya Blatter kutangaza kuwa atajiuzulu wadhifa wake.
Wakati ambao waendesha mashtaka nchini Marekani wanaoifuatilia tuhuma za rushwa walikamata maafisa saba wa Fifa nchini Switzerland kati ya watu 14 wanaotuhumiwa kwenye kashfa hiyo.
Hata hivyo Blatter alisema anatumia mamlaka aliyopewa hata kama hayakubaliwi na kila mtu duniani.
Fifa inahitaji mabadiliko makubwa ili kukemea rushwa.
Mwandishi wa BBC,Nick Bryant mjini New York anasema kuwa bado maafisa hao wa marekani wana matumaini ya kupata ushirikiano kutoka kwenye takwimu za Fifa kwa sasa ili kubaini namna ambavyo mzunguko wa pesa chafu unavyomuhusisha Blatter.
Katika taarifa iliyoripotiwa kutoka kwa maafisa wa Marekani wiki iliyopita kuhusu rushwa katika shirikisho hilo la soka ulimwenguni, Mwanasheria Mkuu wa Serikali Loretta Lynch haikumshutumu Blatter moja kwa moja .
Ingawa alisema kuwa huu ni mwanzo tu wa uchunguzi na si mwisho.
Mwandishi wetu anasema huu ni msingi wa maafisa wa marekani katika kuikomboa dunia katika majanga makubwa kama haya.
Mwanzoni FBI,mamlaka ya ndani ya huduma za Mapato nchini Marekani na mwanasheria wa New York , ambaye alishiriki katika uchunguzi huo walisema kuwa hawana maoni juu ya kujiuzulu kwa Blatter.